top of page

Mama mwenye umri makamo aingia darasani, abobea teknolojia majiko

TABU Kashele, ni mwanamama mwenye umri wa miaka 65, ambaye ana watoto watano. Ana simulizi ya jinsi alivyokuwa akichekwa, pale alipokuwa anatafuta udongo kwa ajili ya kutengeneza majiko.


Hawakujua ni safari ya kiteknolojia, akitafuta malighafi udongo atimize ujuzi wake, ambao mbele unamfanikishia maisha.


Mama Tabu anasema, ni safari ya ujasiriamali ambayo amekutana na changamoto mbalimbali, haikuwa rahisi kutokana na wengine kumzungumzia umri wake umekwenda na kile anachokifanya katika kujitafutia kipato.


Anasema, hakuangalia vikwazo alivyokutana navyo ilikuwa ni kutimiza sura mbili za malengo, anatumikia ujuzi wa kiteknolojia aliyo nayo yenye dhamira ya kuhakikisha anatengeneza majiko bora, yatakayomwingizia kipato, akiwa na soko la ndani na nje ya nchi.


"Watu walikuwa wananicheka umri wangu ni mkubwa  eti nacheza na udongo, mara nimekosa kazi za kufanya sikusikiliza maneno yao. Nilihakikisha natimiza kile ambacho nakitaka kukifanya hata kama umri wangu umeenda," anasema 


NI JIKO AINA GANI?


Tabu anasema jiko analotengeneza lina pembe nne na kando yake ina sehemu ya kutoa mvuke, kunakowekwa kuni moja hata mtu anaweza kupika chai kwa mvuke, unatengeneza vyakula kwa njia ya mvuke.Anasema, jiko hilo halihamishiki na limekuwa likipendwa katika maeneo ya vyuo, tena lisilotumia gharama kubwa katika matumizi yake ya msingi.


Tabu anasema, kuna wakati ilimlazimu kujiongeza na kutengeneza majiko yanayohamishika, ili hata waliopo katika maeneo kama vile mikoa ya mbali wanakoweza kufaidika na huduma hiyo."Nilikaa chini nikajiuliza mtu ambaye yupo Shinyanga atawezaje kulinunua hili jiko? Ikabidi niwe mbunifu na kutengeneza majiko ambayo yanahamishika," anasimulia.


Mteknolojia huyo anasimulia kwamba, majiko yake anayatengeneza kwa kutumia udongo mfinyanzi na baada ya kukamilika, huyachoma na kuyaweka katika mwonekano bora.


Kuhusu namna alivyojisogeza katoka katika ujasiriamali wa kutengeneza majiko hayo, anasema alianza rasmi mwaka 1995 na jiko moja alianza kuuza kwa bei ya Sh. 500, lakini namna yalivyokuwa na mvuto kwa wateja alijikuta ana mauzo ya jumla ya Sh, 50,000, jambo lililomfurahisha maradufu.


LINI WALIANZA?

Mama Tabu anasema ulikuwa mwaka 1992, walipohamasishwa kujifunza kutengeneza majiko yasiyohamishika kutoka kwa raia mmoja wa Kizungu, ambaye hamkumbuki jina lake, alikuwa mkazi wa jijini Mwanza.


Katika mafunzo hayo ya mwaka 1992, anaeleza walipekekwa nchini Kenya kujifunza zaidi na kujionea jinsi watu wanavyotajirika kutokana na majiko aina hiyo ya udongo, jumla yao wakiwa wanafunzi 110. Tabu anafafanua: "Alikuja Mzungu kuhamashisha yale majiko yasiyohamishika tukapelekwa Kenya kuona wenzetu walivyoendelea tulikuta watu wanatajirika kwa ajili ya udongo nilihamasika."


Anasimulia kwamba, ilichukua mwaka mmoja kwa mafunzo hayo kukamilika kwa kupatiwa cheti cha kutengeneza majiko, baada ya hapo aliendelea na shughuli zake za kutengeneza majiko. Mnamo mwaka 2013, alipata wafadhili wanaojulikana kutoka asasi kutoka nchini Canada aliyoitaja kuwa na ofisi mkoani Mwanza. Tabu anaendeleza simulizi kwamba, baada ya kumuona anatumia nguvu kubwa katika utengenezaji majiko, alipatiwa vifaa vya mashine kwa ajili ya kurahisisha kazi yake, kwani awali alitumia mikono.


ALIVYO SASA

Mama huyo anasema, kwa sasa naye ana mashine anayotengeneza kila siku majiko 100 na alishawafundisha wanafunzi 149,000 katika maeneo anayoyataja kuwa ni Simiyu, Mwanza, Bariadi, Morogoro, Kahama pia nchi jirani, zikiwamo Rwanda, Burundi na Uganda.


Anasema, mbali na anaowataja kuna wanafunzi wanaoenda nyumbani kwake kujifunza, hali kadhalika wengine huwafuata katika mikoa waliopo na hadi sasa anaendelea na kazi anayotengeneza majiko aina ya matawi. Mama huyo mtaalamu anasema, aina ya majiko hayo yamempa umaarufu, kwa siku anaweza kuyauza 10 hadi 20 na mengine wakala wake husambaza katika maeneo mbalimbali.


Anasimulia kuna wakati alipatiwa tuzo ya usafiri aina ya Bajaji kutoka kwa wafadhili ili kumwezesha kusambaza bidhaa zake kwa wakati. Pia, anasimulia kwamba, kwenye maonyesho huwa anauza majiko mengi, kila moja akiuza kwa bei ya Sh. 6,000 na jiko lenye matawi makubwa bei yake inafikia Sh. 10,000, huku yale maalum anayoyajenga yanafika bei Sh. 20,000. Kwa mujibu wa mteknolojia huyo, majiko hayo ni ya gharama nafuu zaidi, kwani mtu anatumia mkaa wa Sh. 1,000 kwa siku tatu.


Tabu anasema kwamba, mbali na kutengeneza majiko, pia kuna chupa za chai za udongo zinazotengezwa, inayotumia saa kadhaa pasipo kupooza chakula. Mwanamke huyo anasema, mustakabali wa teknolojia hiyo inafika hatua za kuunda hotipoti, bakuli, vifaa vya kuwekea mishumaa, pasi inayotumia mikaa mitatu pamoja na vikombe vya chai ya udongo anavyovichoma ili visiweze kumong’onyoka.


CHANGAMOTO JE?

Mama huyo anataja upatikanaji wa masoko ni tatizo, akiongeza: "Kuna wateja wengine wanataka kazi na baada ya siku wanakaa kimya hiyo ni changamoto ambayo hainisumbui, nitapambana nitauza kwa wateja wengine." Anasema awali alivyokuwa anachimba udongo, ilikuwa bure, ila sasa walivyogundua udongo una faida, wakaanza kumuuzia.

 

MAISHA YAKE?

Tabu anasema biashara hiyo imemwezesha kupata mafanikio mbalimbali ikiwamo kumiliki nyumba mbili za kisasa. Anasema awali alikuwa ni mama wa nyumbani na biashara hiyo aliianza akiwa ni mtu mzima na kuna watu walifikia hatua ya kumcheka pale alipoonekana akihangaika kubeba udongo ambao ndio malighafi yake.


Pia anataja katika harakati hizo wapo wengi walisoma pamoja katika darasa la teknolijia hiyo, lakini waliiona kazi hiyo ngumu, akajikuta amebaki peke yake aliyeenda kuanzisha mradi wa kutengeneza majiko. Hata hivyo, anakiri kapitia hatua ngumu za kutetea teknolojia na maisha yake kiuchumi, huku akiitaja kuwa sababu mojawapo ya kung’ang’ania mwelekeo huo.


Mama huyo anarejea kwamba, akiwa katika hali ngumu ya kiuchumi aliyokuwa nayo, alipofika nchini Kenya alishuhudia namna wanufaika wa teknolojia hiyo ya udongo walivyonufaika. Hapo katika kufanikisha anachokifanya sasa, anasema hivi sasa anashirikiana na mumewe aliyebeba jukumu la kuyang’arisha na kuyaweka imara majiko hayo anayotegeneza kwa udongo, baada ya kukauka kwa kuyarembesha na kisha anapeleka kuzichoma. “Mume wangu alinipa ushirikiano mkubwa. Tulikuwa tunakwenda wote kuchimba udongo, kwa sasa hatuna shida tunajitosheleza sisi wenyewe. Hatupendi kuwasumbua watoto hata tunapokuwa na changamoto tunajitahidi kujisaidia,” anasema.


Katika kuhitimisha hilo, wameajiri vijana kwa ajili ya uchimbaji udongo na kuponda, huku akiwa katika mchakato wa  kujenga karakana ya kutengenezea majiko ya chuma. Hadi sasa anajivunia mradi wa majiko umempa faida nyingine ya kuanzisha kilimo cha mpunga ekari saba na amenunua ng’ombe 12, pia ana mashamba kadhaa.


WABUNIFU MRADI

Meneja Miradi  wa Mtandao wa Nishati na Jinsia Tanzania (TANGSEN), Thabit Mikidadi, anasema wana lengo la kuona wanawake wengi zaidi wanashiriki katika sekta ya nishati katika ngazi za uamuzi kama wafanyabiashara, vilevile katika ajira na fursa nyingine zinazojitokeza. Anasema TANGSEN inawajengea uwezo wanawake, ili waweze kuitumia nishati hasa ya umeme katika kuzalisha majiko hayo, akifafanua kwamba wanawake wakiwa wengi katika ujasiriamali wa nishati, wanaongeza wigo wa uchumi na kuinua pato la familia.



54 views0 comments

Comments


bottom of page