Makala kutoka nukta.co.tz. Imeandikwa na Rodgers George Agosti 21, 2021
Ni mashine inayochakata unga muhogo kwa saa tatu badala ya siku tatu.
Imewezesha vijana wilayani Mkuranga kujiajiri.
Watakiwa kutumia nishati safi na salama.
Mashine ya kuchakata muhogo inayotumia petroli. Picha na Rodgers George/NUKTA
Dar es Salaam. Katika biashara yeyote, muda kwa ajili ya uzalishaji ni kitu muhimu kuzingatia.
Bila matumizi ya teknolojia ya kisasa, mtu anayezalisha unga wa mhogo, alihitaji kuwa na siku tatu hadi nne ili kuzalisha unga wa muhogo.
Hata hivyo, mapinduzi ya teknolojia yamerahisisha kazi hiyo kwa sababu wabunifu wamebuni mashine ambayo inaweza kutengeneza unga wa muhogo kwa saa tatu tu.
Katibu Mteule wa kikundi cha kulima na kuzalisha mihogo katika Wilaya ya Mkuranga (MCAP) mkoani Pwani, Omari Juma anasema yeye na wana kikundi wenzake 14 wanamiliki mashine hiyo inayowawezesha kuzalisha unga wa muhogo ndani ya muda mfupi.
Licha ya kuzalisha unga wa muhugo, vijana hao wanalima zao hilo ikiwa ni njia ya kuhakikisha wanakuwa na mnyororo wa thamani unaowawezesha kupata kipato kuwawezesha kuendesha familia.
“Zamani tulihitaji siku tatu au zaidi kutengeneza unga wa muhogo, sasahivi ni muda mfupi tu tayari muhogo upo tayari kwenda sokoni. Tena sasa hivi tunafanya kazi bila wasiwasi hata wa kipindi cha mvua” anasema Juma.
Katika baadhi ya jamii, zamani kuchakata mihogo kabla ya kupata unga ilihusisha kuvuna mihogo, kuimenya na kisha kuanikwa juani ili kupunguza maji maji ili iwe rahisi kuvundikwa.
Baada ya kuanikwa juani na kukauka kwa walau saa tatu, mihogo hiyo inahamishiwa ndani kwenye kona ya jiko ambapo inawekwa vizuri na kisha kufunikwa na majani mengi ikiwa ni hatua ya uvundikaji.
Siku tatu baadaye mihogo hutolewa hupondwa pondwa katika vipande vidogo na kisha kuanikwa tena tayari kwa kusagwa ili kupata unga.
Sasa mambo yamebadilika, teknolojia imerahisisha kila kitu.
Undani wa teknolojia hiyo
Mashine inayotumiwa na kikundi cha MCAP imetengenezwa na kampuni ya Intermech Engineering Limited ya mkoani Morogoro ambapo gharama yake ni Sh1.9 milioni.
“Unachagua mfumo ambao unataka mashine iwe. Unaweza kuchagua mashine ya umeme au ya kutumia jenereta. Zote gharama yake ni moja,” amesema mtoa huduma kwa mteja wa kampuni hiyo wakati akiongea na Nukta Habari kwa njia ya simu.
Wana MCAP walichagua mashine ambayo inatumia mafuta kwa sababu bado ofisi yao haijaunganishwa na umeme licha ya nguzo mbili za umeme kuwa umbali wa hatua kumi tu za miguu kutoka ofisini kwao.
Kwa mashine ambayo wamechagua wana kikundi hao, inawagharimu Sh2,600 kwa kila lita ya mafuta wanayoitumia.
Gharama hiyo ni nje ya gharama za maji, kilimo na usafiri wa hapa na pale katika shughuli zao za kuzalisha unga wa muhogo.
Wana kikundi hao huzalisha kilogramu 600 za unga kila baada ya siku tatu au nne kwani soko lao bado ni dogo.
“Hii mashine inatumia mafuta hivyo huwa tunasaga na kuiacha ipumzike. Hatusagi kwa mfululizo,” amesema Juma.
Kwa mujibu wa Juma, mafuta kwa ajili ya mashine yao huwa yanafuatwa kata Kimanzichana iliyopo wilayani humo ambapo nauli ya kwenda na kurudi ni Sh6,000 na mashine yao ikihitaji fundi huwa wanatoa kati ya Sh7,000 na Sh10,000 kwa ajili ya matengenezo.
Uanikaji wa mihogo baada ya kuchakatwa. Picha na TANGSEN
Njia mbadala ya kutumia teknolojia hiyo
Afisa programu kutoka Mtandao wa Jinsia na Nishati Endelevu Tanzania (TANGSEN), Thabit Mikidadi, amesema wanaMCAP wangeliweza kuokoa matumizi makubwa ya fedha kwa kuchagua kutumia mashine inayotumia mfumo wa umeme.
Mikidadi ameiambia Nukta kuwa mashine inayoendeshwa na mafuta, kuna gharama nyingi ambazo zinajitokeza ikiwemo gharama ya usafiri wa kufuata mafuta na mategenezo.
Amesema endapo wanakikundi hao wangelitumia mashine ya umeme ambao upo nje tu ya ofisi yao, wangeliweza kuokoa gharama hizo za mara kwa mara.
“Umeme huwa na bei maalumu walau kwa mwaka mzima. Ni tofauti na petroli ambayo kila mwezi inaweza kuwa na bei mpya,” amesema Mikidadi.
Teknolojia imetengenezwa ili kurahisisha kazi na kuwezesha vitu vigumu kufanyika kwa njia nyepesi na kwa ufanisi. Kutokana na hilo, mara kwa mara wataalam wa masuala ya teknolojia hujitahidi kutengeneza teknolojia zinazoendana na mahitaji ya watu.
Mhandisi Mitambo na teknolojia za nishati jadidifu kutoka Tangsen, Leonard Pesambili amesema changamoto inayowasumbua wana MCAP siyo teknolojia pekee bali uelewa wa uendeshaji wa biashara na masoko.
Mhandisi huyo amesema wakipatiwa elimu nzuri ya masoko itawasaidia kuokoa gharama ambazo wanazitumia katika kuendesha mashine yao na kuzitumia katika kuongeza uzalishaji.
“Matumizi ya petroli yanaambatana na uchafuzi wa mazingira lakini umeme sio tu ni ahueni hasa kwa hali ya kikundi chao lakini pia utawaongezea kasi ya uzalishaji huku ukiwa ni rafiki kwa mazingira,” amesema Mhandisi Pesambili.
Wataalam hao wanaeleza kuwa umeme ni nishati safi na salama ambayo inapunguza uharibifu wa mazingira.
Comments