Dar es Salaam. Hamasa ya wasichana kujikita katika masomo ya sayansi imeendelea kupata msukumo kwa wadau mbalimbali kutafuta njia mbadala za kuhakikisha wasichana wanaingia kwa wingi katika masomo hayo ili kupata wataalam wengi wa kike. Leo ikiwa ni Siku ya Wanawake Duniani, yapo mengi ya kujivunia kwa wadau hasa wanawake ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwainua wasichana kwa maarifa na ujuzi hasa kwenye nyanja ya teknolojia. Mwandishi wa vitabu, Getrude Mligo ni mmoja wa wadau hao ambaye anatumia talanta yake ya uandishi wa vitabu kuwafikia wasichana mashuleni kwa lengo la kuwahamasisha kutokukatia tamaa masomo ya sayansi ili baadaye waikomboe jamii kwa kufanya yale yanayosemekana kutokufanywa na wanawake.
“Wakati nasoma, madarasa ya sayansi yalikuwa wamejaa wavulana. Ukimwambia mtu kuwa una mpango wa kusoma fizikia, kemia na hesabu, utasikia anakuambia huwezi kwa sababu wewe ni msichana. Hiyo ni kati ya sababu za kutokuwa na wanawake wengi wanasayansi,” amesema Mligo. Binti huyo alichagua masomo ya Uchumi, Jografia na Hesabu (EGM) wakati akisoma elimu ya sekondari na katika mazungumzo yake na Nukta, amesema baba yake ndiyo alikua nguzo ya kuegemea kwa kuwa alikuwa akimhamasisha kufanya vitu alivyodhani ni vigumu ikiwemo somo la hesabu na Jografia.
“Kwa sasa mimi ni mwandishi wa vitabu na mwanaharakati wa haki za wanawake na wasichana. Kama mwandishi, natumia talanta kuambukiza tabia chanya wasichana waliopo mashuleni na wanawake katika jamii,” anasema binti huyo ambaye ana Shahada ya Menejimenti ya rasilimali watu. Sababu hiyo ndiyo iliyomfanya mwandishi huyo kuanza safari ya kuandika vitabu vya kuhamasisha wasichana kujihusisha na masomo ambayo mara nyingi husemekana kuwa kazi zake ni za wanaume ikiwemo uhandisi na udaktari.
Moja ya kitabu alichoandika binti huyo kinajulikana kama "Wasichana Waliogundua Umeme wa Upepo" ametumia mfano wa namna wasichana wanaweza kugundua njia rahisi za teknolojia kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii. “Katika kitabu changu cha Wasichana waliogundua umeme wa upepo, ninetumia wahusika walio na uhalisia ili kuwapatia motisha wasichana,” amesema Getrude. Mligo ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa wasichana hao pia walikatishwa tamaa na kubezwa juu ya masomi waliyochukua na kuambiwa kuwa “hayawapendezi” kusoma kama wasichana.
Katika kitabu hicho, ametumia wahusika wakiwemo Tausi Ibrahim (rubani), Julieth Seba (Daktari), Zainab Hassan (mhasibu) Hellen Kidato (mwanasayansi wa mimea).
Kitabu hicho kimetolewa kopi 600 ambazo zinagawiwa bure kwa wanafunzi mashuleni huku watu wengine wakikinunua kwa Sh10,000 inayotumika kuzalisha vitabu vingine ili kuwafikia wasichana wengi zaidi mashuleni.
Kwanini kitabu hicho?
Kitabu cha Mligo kimehusisha umeme wa upepo ambao ni umeme safi na jadidifu. Licha ya kuwa Tanzania tayari inazalisha umeme huo Makambako mkoani Njombe, binti huyo amesema anaamini kupitia kitabu chake, wasichana watatoka katika hali ya mazoea na kufanya vitu vikubwa zaidi na kujihusisha na umeme ambao ni salama kwa mazingira na hata kwa kupikia.
Getrude ambaye amekuwa akionekana katika majukwaa mbalimbali ya wanawake anasema ameamua kutumia simulizi ya umeme wa upepo kwa sababu licha ya umuhimu wake katika usafi wa mazingira, bado umeme huo hauongelewi sana. Kwa kuliona hilo, anasema kitabu chake kitaanza kuchochea moto kwa wasichana mashuleni kuanza kuangazia mambo ambayo yanaonekana kuwa ni magumu.
“Msichana ni kama jiko la gesi ambalo limezima. Kwa kuwa haliwaki, haimaanishi kuwa halifanyi kazi, unapoliwasha na kuweka kiberiti ndipo utaona linawaka na moto wake ni mkubwa. Ninaamini kitabu hiki kitawasha moto miongoni mwa wasichana,” anasisitiza.
Kitabu hicho kinaelezea hadithi ya wasichana waliobuni umeme wa upepo ili kukomboa kijiji chao. Kimeonyesha kuwa jinsia sio kigezo cha kufanya mambo makubwa hasa ya kisayansi.
Kwa sasa, Getrude amesema kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na kinapatikana kwa mfumo wa chapisho pamoja na kwa njia ya mtandao kupitia mtandao wa Amazon.
"Tunampango wa kukiweka katika njia ya sauti na kukitafsiri kwa lugha ya Kiingereza ili kuwafikia watu wengi zaidi," amesema Mligo.
Mbali na kitabu cha “Wasichana waliogundua umeme wa upepo” pia ameandika kitabu cha “Dear Girl Child” cha mwaka 2020 ambacho kinafundisha wasichana juu ya kupaza sauti juu ya ukatili wa kijinsia ambao unawakuta katika maisha ya kila siku.
Kitabu hicho kinalenga kumwezesha msichana kufanya maamuzi sahihi kwa sababu baadhi yao wanapitia ukatili wa kijinsia lakini wanashindwa kutoa taarifa ili wapate msaada.
Dear Girl Child kilitolewa kopi 700 ambazo zilisambazwa katika shule mbalimbali nchini Tanzania na ili maktaba ili kufikiwa na kila aliyehitaji kukisoma.
“Tulipeleka vitabu shule nyingi lakini wanafunzi zaidi ya 10 waliturudia wakisema kitabu kimewaelimisha na wamepata nguvu ya kuanika waliyokuwa wakifanyiwa,” anaeleza Getrude.
Kuna kila sababu ya kuwahamasisha wasichana kusoma vitabu wakiwa shuleni hasa vile vinavyowapa hamasa ya kuwa bora zaidi na kuwafanya watimize ndoto zao za kielimu.
Comments